Sunday, July 16, 2017

Rais Magufuli Ampa pole mwakyembe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison George Mwakyembe kufuatia kifo cha mkewe Bi. Linah George Mwakyembe kilichotokea usiku wa tarehe 15 Julai, 2017.

Bi. Linah George Mwakyembe amefariki dunia katika hospitali ya Agha Khan Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kushtushwa na kusikitishwa na kifo hicho, na amesema yeye na familia yake wanaungana na familia ya Dkt. Mwakyembe katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

“Nakupa pole sana Dkt. Mwakyembe kwa kuondokewa na mkeo mpendwa Bi. Linah, natambua hisia za maumivu ulizonazo wewe na familia nzima, nyote nawaombea Mwenyezi Mungu awatie nguvu, awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

"Namuombea Marehemu Linah George Mwakyembe apumzishwe mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

No comments:

Post a Comment